SIMBA YATUA DAR, KOCHA AOMBA MSAMAHA, AUTAJA MFUMO WA 3-5-2
SIKU moja baada ya kikosi cha Simba kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo Masoud Djuma, amewataka mashabiki wao wasahau yaliyopita na sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom.
Simba ilifungishwa virago mapema katika hatua ya makundi baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0, kutoka kwa URA ya Uganda na kufanya timu
hiyo kusalia katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi zao nne katika mechi nne ilizocheza kwenye michuano hiyo.
Djuma amesema kuwa mfumo alioutumia ulikuwa ni tatizo kwa wachezaji wake na ndiyo maana
wakashindwa kufanya vizuri kwenye michuano hiyo na kujikuta wakiaga mapema kwenye hatua za makundi.
"Niwaombe msamaha wapenzi na wanachama wa Simba, kwa kushindwa kufanya vizuri lakini naomba wasivunjike moyo wanendelee kutupa sapoti kwani
bado tuna kazi ya kutafuta ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na michuano ya kimataifa kote huko tumekusudia kufanya vizuri,"amesema Djuma.
Kocha huyo alisema pamoja na mfumo wa 3-5-2, kuwasumbua wachezaji wake lakini ataendelea kuutumia kwenye mechi zao za ligi na michuano ya kimataifa kwasababu anaamini hadi kufikia kipindi hicho wachezaji wake watakuwa wameshauelewa.
"Tutaufanyia sana mazoezi kila siku kwasababu nimfumo mzuri ambao unatufanya tuwe salama na adui kutokana na kasi ya mashambulizi
tunayopeleka kwenye lango la wapinzani na hata kwenye mchezo na URA pamoja na Azam pamoja na kufungwa lakini tulishambulia sana lakini hatukuweza kuzitumia nafasi tulizotengeneza," alisema kocha huyo.
Comments
Post a Comment