AZAM FC YATAMBA KUWA ITAISHANGAZA SIMBA KWA KUTWAA UBINGWA VPL
Azam FC imeeleza kuwa ipo kwenye mbio za kimya kimya katika kuwania taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na kudai wataishangaza Simba kwa kutwaa ubingwa huo mwishoni mwa msimu huu 2017/2018.
Hadi ligi hiyo ikiwa imemaliza raundi ya 14, Azam FC na Simba zimeonakana kuwa katika mbio kali za kuwania ubingwa wa ligi hiyo, matajiri hao wakishika nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na pointi 30 wakizidiwa pointi mbili na Simba iliyokileleni baada ya kujikusanyia 32.
Kauli hiyo imetolewa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Abdul Mohamed, wakati Azam FC ikiingia mkataba mpya wa mwaka mmoja na wadhamini wakuu Benki ya NMB na kuungwa mkono na Meneja wa timu, Phillip Alando.
“Kwa sasa tuko katika mbio za kimyakimya, zisizo na tambo nyingi, tukiongozwa na dhamira ya dhati ya kutwaa taji hilo la ligi, tutalipa fadhila za kuaminiwa huku na NMB kwa kutwaa taji la VPL, kwa sababu Azam FC inaamini katika mafanikio kama kichocheo cha kuvutia wadhaamini wengine,” alisema Mohamed.
Kwa upande wake, Meneja Alando alisema kuwa hawana muda tena wa kutoa tambo, badala yake wanapambana kimyakimya kuhakikisha wanawashangaza wapinzani wao Simba na kujinasibu mwisho wa msimu watamaliza kileleni na kutwaa taji hilo.
Kikosi cha Azam FC kwa sasa kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mchezo ujao wa ligi dhidi ya Yanga, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumamosi hii.
Comments
Post a Comment