MBAO FC WAPIGWA TENA NA RUVU SHOOTING
Mabao mawili ya Khamis Mcha ‘Vialli’ jioni ya leo yametosha kuipa Ruvu Shooting ushindi wa 2-0 dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Mcha, kiungo mshambuliaji aliyeshinda taji la Ligi Kuu na Azam FC msimu wa 2013-2014, alifunga mabao yake katika dakika za 26 na 44.
Na sasa Ruvu Shooting inafikisha pointi 14 na kupanda hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kucheza mechi 15, wakati Mbao FC inabaki nafasi ya nane kwa pointi zake 15 za mechi 15.
Mzunguko wa 15 wa Ligi Kuu utaendelea kesho kwa mechi nne; Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Njombe Mji FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Azam FC wataikaribisha Yanga SC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Mbeya City watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Kagera Sugar wataialika Lipuli FC Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Duru la kwanza la Ligi Kuu litakamilishwa Jumapili kwa mechi mbili, vinara Simba SC wakimenyana na Maji Maji FC ya Songea Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na Singida United watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Namfua mkoani Singida.
Comments
Post a Comment