AZAM FC UWANJANI LEO KUKIPIGA DHIDI YA SHUPAVU FC
Kikosi cha Azam FC kiliwasili salama mkoani Morogoro kwa ajili ya kuvaana na Shupavu katika mchezo wa raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, leo Jumanne saa 8.00 mchana.
Mara baada ya kuwasili jana mchana na kufikia katika Hoteli ya Oasis, kikosi hicho kilifanya mazoezi ya mwisho jana jioni kwenye uwanja huo utakaochezewa mechi, ambapo huenda benchi la ufundi likakifanyia mabadiliko madogo kikosi kitakachoanza kwa kuwapumzisha baadhi ya wachezaji.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, amesema kuwa wanauchukulia uzito mchezo huo kwa kuhakikisha wanashinda kutokana na bingwa wa michuano hiyo kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika (CC).
“Kwa malengo hayo tumeuweka huu mchezo kwa kupambana kwa asilimia 100, na ndio maana toka vijana wetu wamemaliza mchezo uliopita dhidi ya Yanga wameendelea kukaa kambini ili kuhakikisha wapo salama na wanajiandaa tayari kupambana na wapinzani wetu Shupavu,” alisema.
Azam FC itaingia kwenye mchezo huo dhidi ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara (SDL) ikiwa na kumbukumbu ya kuitoa Area C United ya Dodoma kwa mabao 4-0, yaliyofungwa na kiungo Salmin Hoza, Nahodha Msaidizi Agrey Moris, Yahya Zayd na Enock Atta.
Comments
Post a Comment