OKWI AKIZUBAA ITAKULA KWAKE
KAIMU kocha mkuu wa Simba, Djuma Masoud, amesema mchezaji atakayepata namba kwenye kikosi chake ni yule atakayejitoa kisawasawa kuanzia mazoezini, hiyo ikimaanisha kuwa straika Mganda anayesumbua, Emmanuel Okwi, anatakiwa kuweka masihara pembeni na kufanya kazi, vinginevyo imekula kwake.
Akizungumza na DIMBA jana, Masoud alisema anatoa nafasi kwa mchezaji ambaye ataonyesha kiwango kizuri na hataangalia jina au umaarufu wa mtu.
Alisema mpango wake ni kuhakikisha kila mchezaji anakuwa na uwezo mkubwa ili kuwepo na changamoto za namba na kuwa na kikosi imara hivyo atakayejiona mkubwa kuliko timu atajikuta akisugulishwa benchi.
“Hakuna kuangalia jina, hapa ni kiwango cha mchezaji ndicho kitambeba, nadhani kila kocha anatamani kuona wachezaji wake wakijituma,” alisema.
Okwi hakuonekana katika baadhi ya michezo ikiwamo ya Mapinduzi inayoendelea Zanzibar, kutokana na sababu mbalimbali lakini atatakiwa kujituma atakaporejea kwani Masoud hana masihara.
Okwi ndiye anayeongoza katika ufungaji Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwa na mabao nane, huku akikosa michezo ya mwisho ikiwamo ule dhidi ya Ndanda FC, Simba ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Comments
Post a Comment