HIZI NDIYO REKODI ZA TANZANIA PRISONS VS AZAM FC



Kuelekea mchezo wa Tanzania Prisons dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Sokoine kuna mambo kadhaa yanahohusu mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom utakaopigwa leo Jumapili.
Rekodi zinaonyesha kuwa hadi sasa, kihistoria timu hizo zimekutana mara 14 kwenye mechi za ligi, Azam FC ikiwa na rekodi ya kushinda mara tano, Prisons yenyewe mara tatu ikiibuka kidedea huku ikishuhudiwa mechi sita zikiisha kwa sare.
Azam FC ambayo inauchukulia kwa uzito mkubwa mchezo huo hasa ikitaka kuifikia Simba kwenye mbio za ubingwa, ilipata ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa mwisho uliofanyika uwanjani hapo msimu uliopita.
Bao pekee la Azam FC lilifungwa kiustadi kwa shuti na aliyekuwa kiungo mkabaji wa timu hiyo, Michael Bolou, bao lililofanya rekodi kuandikwa upya kwa mabingwa hao kupata ushindi wa kwanza Sokoine dhidi ya Prisons kwenye mechi saba walizocheza ndani ya dimba hilo.
Ukiondoa mechi moja ambayo Azam FC imeitambia Prisons, mechi nyingine sita zilizobakia zilizopigwa mjini Mbeya, maafande hao wameshinda mara mbili huku nne zikiisha kwa sare.
Jumla ya mabao 22 yamefungwa na timu hizo katika mechi zote 14 walizokutana, Azam FC imefunga 12 (nusu ya mabao yote) na Prisons ikitupia 10 tu kwenye nyavu za mabingwa hao wa ligi msimu 2013/2014.
Ushindi wowote kesho utaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 30 kwenye msimamo wa ligi na kukaa kileleni kwa muda ikisubiria matokea ya Simba itakayocheza na Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba keshokutwa Jumatatu.

Comments

Popular posts from this blog

Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!