WAAMUZI WAMEFIKIA HATUA YA KUHARIBU UTAMU WA LIGI
TAYARI tumeshashuhudia viwanja kadhaa hapa nchini mechi za Ligi Kuu Bara kwa msimu huu zikichezwa. Ni kwa muda mrefu burudani hiyo ya soka ilikuwa ikisubiriwa.
Timu 20 zimeanza kuonyesha uwezo wao ambapo baadhi yao zimecheza mechi mbili tayari huku zingine zikishuka dimbani mara moja.
Muamko wa mashabiki kwenda viwanjani bado hauridhishi kwani wengi wao wameamua kubaki kuangalia kwenye runinga, kuna umuhimu pia kwa mashabiki kuweza kufika katika viwanja kutoa sapoti kwa timu zao.
Kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kuweza kujenga imani na hali ya kujituma zaidi kwa wachezaji kwa lengo la kupata matokeo mazuri kwa kuwa uwepo wa mashabiki, wachezaji wanapata nguvu ya kupambana.
Mambo mengi yanayotokea katika ligi hiyo ambayo inaendelea, kuna umuhimu wa kuchukua hatua mapema kwa yale ambayo si sahihi kabla ya matukio mengine makubwa hayajawa sugu wakati ligi ikiendelea.
Kabla sijakupeleka kwenye jamvi la leo, kuna umuhimu wa kuweza kuwapongeza vijana wetu wa Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys, ambao wameshiriki mashindano ya kufuzu kwa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika chini ya umri huo (Afcon U17) kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambayo yalikuwa yana mvuto wa kipekee.
Ninachotaka kusema ni kwamba muda huu ni lazima Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liweze kuweka mikakati maalumu ya kuwatunza hawa vijana ili siku za usoni waweze kutumika kwenye timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars.
Kwa kuweza kuwekeza kwa hawa vijana kutafanya tuwe na kizazi ambacho kitakuwa na ushindani hasa kwenye mashindano ya kimataifa kwa kuwa tayari wana kitu cha kipekee walichonacho.
Tusikubali tukawapoteza kwani kwa kufanya hivyo hakutakuwa na maana yoyote ile hasa kwa maendeleo ya soka letu hapo baadaye kwa kuwa ni kizazi ambacho kinafundishika na kinaweza kuwa na manufaa makubwa kwetu sote.
Nikirudi kwenye kile nilicholenga kukisema ni kwamba, katika mechi za awali zilizochezwa mpaka sasa, kuna malalamiko yamejitokeza kwa baadhi ya waamuzi juu ya uamuzi wao.
Tutambue kuwa vile utakavyoanza ndivyo utakavyomaliza, ni muhimu kutatua mapema tatizo ambalo lipo ili kuendelea na ligi itakayokuwa na ushindani na sio maneno kila siku.
Waamuzi wameonekana kuanza na makosa ambayo yamejitokeza waziwazi na kila mmoja ameyaona.
Jambo la kushangaza sana ni kwamba, waamuzi hao wengi wamefanya makosa ambayo yanafana kuhusiana na kutatua sheria ya kuotea.
Inapotokea timu imenyimwa haki yake, makocha, wachezaji na hata viongozi wa timu huwa kwenye maumivu makubwa jambo ambalo linawakatisha tamaa.
Mfano wa wazi ni katika mechi ya Coastal Union dhidi ya Biashara, mwamuzi alikataa bao lililofungwa kwa njia ya faulo na Biashara hali ambayo inaleta maswali ambayo mengi hayana majibu.
Pia hata ile mechi ya Ruvu Shooting dhidi ya KMC, tuliona kwamba kuna bao lilifungwa na Ruvu Shooting nalo lilikataliwa kwa madai kwamba mfungaji kabla ya kufunga, alikuwa ameotea.
Inafahamika wazi kwamba waamuzi nao ni binadamu kama walivyo wengine, hivyo kuna kupitiwa, lakini kuna mambo mengine yanayojitokeza yanakera sana kwa sababu huwa yanajirudiarudia.
Sitaki kuhusisha ishu hizi na mambo ya rushwa, bali ninachotaka kusema ni kwamba, tunahitaji umakini katika kila idara ili kuifanya ligi yetu iwe na ushindani mkubwa.
Kigezo cha kukosekana kwa mdhamini mkuu kisitumike kwa baadhi ya timu kuanza kununua mechi, kama kuna timu zinafanya hivyo zitakuwa zinakosea sana.
Kumekuwa na dhana kwamba kwa timu ambazo zina uwezo wa kifedha ni rahisi kutengeneza mazingira ya kushinda mechi zake kwa njia yoyote ile jambo ambalo halikuzi soka letu bali linazidi kudidimiza.
Kama Shrikisho la Soka Tanzania (TFF) litakubali ligi kuendelea hivi bila ya kuwa na mdhamini kuna mambo mengi ya ajabu tutayashuhudia msimu huu ambayo yatashusha hadhi ya ligi yenyewe.
Suala la rushwa litazungumzwa sana msimu huu kwa kuwa kutakuwa na dalili nyingi juu ya suala hilo, hivyo ili kuweza kujiepusha katika hili kuna umuhimu wa kuweza kutafuta mdhamini ambaye ataweza kuzipa nguvu klabu katika kujiendesha na kuifanya ligi kuwa na ushindani wa kweli.
Kwa mazingira ambayo tunayapitia kwa sasa kuna uwezekano mkubwa sana kila timu itakaposhindwa ikaanza kuwashushia lawama waamuzi kwa kuwa tayari wameanza kuonyesha dalili ambazo zinaleta mashaka na kuwahusisha na masuala ya rushwa.
Pia msimu huu nadhani hakutakuwa na ule msisimko ambao uliweza kuonekana msimu uliopita kutokana na ukweli kwamba timu nyingi ambazo zinashiriki ligi hazina mdhamini zaidi zinajiendesha zenyewe na suala la kuendesha klabu tunatambua kwamba si jambo dogo
Comments
Post a Comment