HABARI ZA KITAIFA DONALD NGOMA APEWA PROGRAMU MAALUM YA MAZOEZI NCHINI UGANDA



Mshambuliaji wa Azam FC, Donald Ngoma, anaendelea na programu maalum ya mazoezi mepesi aliyopewa kabla ya kurejea uwanjani wiki ijayo.
Nyota huyo raia wa Zimbabwe anaendelea vizuri akiwa kwenye hatua za mwisho ya kurejea uwanjani, ambapo awali wataalamu wa Hospitali ya Vincent Pallotti, Cape Town, Afrika Kusini walimpatia matibabu walibaini Ngoma kuchana mtulinga wa mbele wa goti la mguu wa kulia (Anterior Cruciate Ligament).
Wataalamu hao walitoa ripoti ya nyota huyo kupumzika kwa wiki tisa na kushauri aanze rasmi kucheza mechi ya ushindani kuanzia Agosti 11 mwaka huu, hivi sasa akiwa amebakiza takribani siku 10 kutimia muda huo.
Daktari Mkuu wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, amesema kuwa Ngoma kwa sasa anafanya mazoezi mepesi ya kuimarisha sehemu ya jeraha aliloumia (ligament).
“Wote mnafahamu kwamba Ngoma (Donald) alikwenda kufanyiwa matibabu Afrika Kusini na ameshaanza programu zake za mazoezi (mepesi) kuweza kuimarisha ‘ligament’ (mtulinga wa mbele) iliyokuwa imeumia na sasa yuko kwenye hatua za kupona anafanya mazoezi ya kuimarisha misuli ya paja.
“Na tunatarajia kwamba Ngoma wiki ya pili ya mwezi huu (Agosti) ataweza kucheza kama kawaida na wachezaji wengine,” alisema Dr. Mwankemwa, alipozungumzia maendeleo ya mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Mzimbabwe Donald Ngoma.
Mbali na kufanya mazoezi mepesi ya uwanjani, muda pia muda wowote kuanzia sasa ataanza kujiweka fiti zaidi kwa aina nyingine ya mazoezi kupitia ‘gym’ kwa mujibu ya programu aliyoachiwa alipokwenda Afrika Kusini.
Mchezaji mwingine majeruhi wa Azam FC aliyeko nchini Uganda, winga Joseph Kimwaga, tayari ameruhusiwa kujiunga na wenzake tokea mazoezi ya jana akiwa amepona majeraha ya nyonga yaliyokuwa yakimkabili.
Yakubu je?
Akizungumzia maendeleo ya beki Yakubu Mohammed, mwenye maumivu nyuma ya kifundo cha mguu wa kulia, alisema anatarajia kufanyiwa kipimo cha MRI kwenye Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam ili kubaini undani wa tatizo hilo.
“Yakubu wote mnafahamu kwamba alivunjika mguu mwezi wa pili na alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mwananyamala na baadaye Afrika Kusini (Vincent Pallotti) alikwenda kufanyiwa ‘scan’ kwenye mguu wake wa kulia na kuonekana kwa asilimia 95 ule mfupa umepona.
“Tulitarajia Yakubu aanze mazoezi Juni 5 lakini sasa kwa bahati mbaya sana ni kwamba bado lile eneo la majeraha lina maumivu makali na tukafikiria labda ana tatizo la ligament au misuli kwa hiyo amebaki Tanzania chini ya uangalizi na atapelekwa TMJ Hospital kwa Dr. Faya ambapo atafanyiwa uchunguzi tena pamoja na MRI na kuweza kujua hatima yake,” alisema.

Comments

Popular posts from this blog

Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!