BEKI PRISONS: KAGERE NI HABARI NYINGINE
BAADA ya juzi Jumatano mshambuliaji wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere kuifungia timu hiyo bao la ushindi dhidi ya Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, ametabiriwa kuwa ndiye atakayeibuka mfungaji bora msimu huu.
Juzi Jumatano, Kagere aliiongoza Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Prisons katika mchezo wa ligi kuu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Ijumaa, beki wa kulia wa Prisons, Salum Kimenya ambaye katika mechi hiyo alichezeshwa kama kiungo mshambuliaji anayetokea upande wa kulia, alisema:
“Napenda kumpongeza Kagere kwa kuitumia vizuri nafasi aliyopata kwani hakutaka kuremba, alipopata mpira aliweza kupiga shuti na kufunga goli, ameonyesha kuwa yupo vizuri kiakili lakini pia kimwili.
“Kama angekuwa mchezaji mwingine angejizungusha-zungusha na mwisho tungefika na kumpokonya mpira, kutokana na hali hiyo namtabiria kuwa anaweza kuibuka mfungaji bora kwani nimekuwa nikimfuatilia pia katika mechi nyingine ambazo ameitumikia Simba tangu alipojiunga nayo.”
Comments
Post a Comment