PLUIJM ATAKA KUSHINDA MECHI ZOTE
KOCHA mkuu wa timu ya Azam FC, Hans van Der Pluijm, amesema kuwa mipango yake kwa sasa ni kuhakikisha kwamba wanafanikiwa kushinda mechi zote za ligi kuu ili kuweza kuibuka na ubingwa.
Azam wamefanikiwa kushinda mchezo wa pili katika uwanja wa nyumbani Chamazi ambao mchezo wa kwanza walicheza dhidi ya Mbeya City na kushinda kwa mabao 2-0 na mchezo wa pili ni dhidi ya Ndanda walishinda mabao 3-0.
Akizungumza na Championi Jumatano, Pluijm alisema kuwa anashangazwa na uwezo wa wachezaji wake wakiwa uwanjani jambo ambalo ana imani kwamba litakuwa na matokeo mazuri katika michezo yao ya ligi kuu.
“Malengo yetu ni kuhakikisha kwamba tunafanikiwa kushinda mechi zote ambazo tutacheza nyumbani na ugenini ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuweza kuibuka na ushindi kwa kuwa hakuna mwalimu ambaye anafikiria kufungwa.
“Nidhamu kwa wachezaji na ushirikiano ni kitu muhimu ambacho kinatupa nafasi ya kushinda kwa kuwa ushindani kwa sasa ni mkubwa baada ya timu kuongezeka ila hilo halitupi tabu kwa kuwa huwa ninaongea na wachezaji namna itakayosaidia kuweza kupata matokeo mazuri,” alisema Pluijm.
Azam wamefanikiwa kushinda michezo yao yote miwili dhidi ya Ndanda na Mbeya City ambayo yote imepigwa Dimba la Chamazi.
Comments
Post a Comment