YANGA YATEKETEZA MAMILIONI MWANZA



YANGA imeendelea kuonyesha jeuri ya fedha, ni baada ya jana kutumia usafiri wa ndege kuwafuata wapinzani wao Kagera Sugar mkoani Kagera na ikiwa Mwanza kwa siku moja tu wametumia zaidi ya Sh milioni tatu.
Yanga ilifika Mwanza Jumanne ambapo walipata msosi na siku hiyohiyo waliondoka jijini hapo kwa basi la kukodi kwenda Shinyanga kuwavaa Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

Baada ya kucheza mechi Alhamisi na kupata ushindi wa mabao 2-1, siku hiyohiyo usiku walirejea tena Mwanza wakiwa na basi la kukodi ambapo walikwenda kufikia kwenye hoteli kubwa ya The Pigeon ambapo walilala.
Asubuhi yake wachezaji na benchi la ufundi walipata chakula na huduma zingine ambapo mpaka wanaondoka jana asubuhi kwenda mkoani Kagera, huku nyuma walikuwa wameteketeza zaidi ya milioni tatu.

Hata hivyo pamoja na klabu hiyo kukumbwa na ukata, waliamua kutumia usafiri wa ndege ya Bombadier kutoka Mwanza hadi Kagera kwa ajili ya mechi ya kesho Jumapili ya ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar itakayopigwa Uwanja wa Kaitaba mjini hapo.
Hii ni mara ya pili msimu huu kwa Yanga kupanda ndege kwenye mechi zake za mikoani, awali walipanda walipotoka jijini Dar kuifuata Mwadui FC wakitumia Ndege ya Air Tanzania na kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Akizungumza na Championi Jumamosi, meneja wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema walitoka Shinyanga kwa basi juzi usiku baada ya mchezo wa Mwadui kumalizika kwa Yanga kushinda 2-1 na kulala kwenye hoteli kubwa ya The Pigeon na jana asubuhi kuanza safari ya kwenda Bukoba.

Cannavaro alisema, walitoka Mwanza saa moja kamili asubuhi na kufika Bukoba baada ya nusu saa wakitumia ndege aina ya Bombadier na kuingia kambini kwa ajili ya mchezo dhidi ya Kagera.
Aliongeza kuwa, wakiwa Bukoba watafanya mazoezi kwa siku mbili, juzi Ijumaa na jana Jumamosi kwenye Uwanja wa Kaitaba kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo ambao wanahitaji pointi tatu pekee.

“Kwanza nianze kwa kuwapongeza wachezaji wetu kwa kuipambania timu na kufanikiwa kupata ushindi, ndiyo kitu tulichokuwa tunakihitaji katika mchezo na Mwadui, hivyo nguvu zetu tumezielekeza kwenye mchezo na Kagera ambao ni muhimu kwetu kupata ushindi.

“Katika kutambua umuhimu wa mchezo huu, tumetumia usafiri wa ndege aina ya Bombadier ili kuhakikisha wachezaji hawachoki na safari ili kuhakikisha wanakuwa tayari na mchezo huo dhidi ya Kagera na tulitumia nusu saa kufika hapa Bukoba vijana wetu wakiwa wapo vizuri.

“Hivyo, leo (jana) na kesho (leo) tutafanya mazoezi hapa Bukoba kwa ajili ya wachezaji wetu kuzoeana na kuendana na hali ya hewa tuliyoikuta ambayo ni ya baridi, tunafahamu umuhimu wa mchezo huu, hivyo ni lazima tushinde ili tupunguze idadi ya pointi walizonazo wapinzani wetu Azam FC walio kileleni,” alisema Cannavaro.

Makambo atamba kushinda kila mechi
Baada ya kufunga bao kwenye mechi dhidi ya Mwadui FC, juzi, mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo raia wa DR Congo amesema sasa watapambana kuhakikisha wanapata ushindi kila mechi inayofuata.

“Kazi yangu ninapokuwa Yanga ni kucheza na kufunga hivyo kama kocha atanipa nafasi nitajituma zaidi ili timu yangu iweze kupata matokeo katika kila mchezo ambao tunacheza, uliona Mwadui walivyokuwa wakicheza vizuri na sisi tuliliona hilo na tukajituma na tukapata ushindi, tutafanya hivyo kila mechi.

“Kama kocha atanipanga katika mchezo ujao nitajituma kadiri niwezavyo ili nifunge na timu yangu iweze kupata pointi tatu muhimu,” alisema Makambo mwenye mabao matano.
Wilbert Molandi Dar na Johnson James, Shinyanga.

Comments

Popular posts from this blog

Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!