MBELGIJI SIMBA: NIMEPEWA JINA LA ULIMWENGU
KOCHA wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems ameweka wazi kuwa amekabidhiwa jina la mshambuliaji Thomas Ulimwengu.
Ulimwengu ambaye amevunja mkataba wake na Al Hilal ya Sudan anatajwa kutakiwa na Simba kwa ajili ya kumtumia kwenye michuano ya kimataifa.
Mshambuliaji huyo alikuwa na Taifa Stars nchini Lesotho katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Afrika lakini hakuweza kucheza kutokana na kocha mkuu wa timu hiyo, Mnigeria, Emmanuel Amunike kumuweka benchi.
Ulimwengu amecheza mechi mbili tu chini ya Amunike ambazo zilikuwa ni dhidi ya Uganda na ile mechi ya kwanza ya Cape Verde, hivyo Mbelgiji alitegemea amuone akicheza na Lesotho lakini haikuwa hivyo.
Awali chanzo makini kutoka ndani ya Simba, kililiambia Championi Jumamosi kuwa, klabu hiyo ilikuwa kwenye mchakato wa kutaka kumsaini lakini kwa sasa inaonekana kama unaelekea kukwama kutokana na kocha kutomuona Ulimwengu akicheza licha ya kuambiwa ni mchezaji mzuri.
“Usajili wa Ulimwengu bado haueleweki kwa kuwa kocha alitoa mapendekezo yake kwa kuwa hajamuona akicheza licha ya kuona ‘CV’ kubwa lakini haiwezi kusaidia kutokana na kukaa bila timu kwa kipindi kirefu kabla ya kutua Sudan ambapo amevunja mkataba wake, lakini lolote linaweza kutokea kutoka kwa uongozi wa juu,” alisema mtoa taarifa.
Championi lilimtafuta Aussems ambapo alikiri kupewa jina la Ulimwengu na viongozi wa Simba ili amuangalie kama atafaa kwenye kikosi chake lakini alisema: “Kuhusu huyo mchezaji nimeshapewa jina lake lakini siwezi kufanya maamuzi yoyote kwa kuwa sijamuona vizuri akicheza.”
Ibrahim Mussa, Dar es Salaam
Comments
Post a Comment