Samatta awafunika nyota Arsenal, Chelsea




Dar es Salaam. Wakati akizidi kuchochea kasi ya kuwania kiatu cha dhahabu kwenye Ligi Kuu ya Ubelgiji, nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta (26), amewafunika mastaa wanne wa klabu kubwa za England, Arsenal na Chelsea.
Wachezaji hao maarufu ni Pierre-Emerick Aubameyang, Olivier Giroud, Danny Welbeck, Alexandre Lacazette wanaocheza Arsenal na Alvaro Morata wa Chelsea.
Mastaa hao wameshindwa kufua dafu mbele ya Samatta katika orodha ya nyota wanaofanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Europa yanayoshika nafasi ya pili kwa ukubwa kwenye ngazi ya klabu Ulaya.
Rekodi zilizotolewa na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), Samatta ameingia katika orodha ya nyota 10 bora waliofanya vizuri katika mashindano hayo hadi hivi sasa kutokana na ufanisi mkubwa alioonyesha kwenye Ligi ya Europa akiwa na kikosi cha KRC Genk.
Wakati akishika nafasi ya 10 katika orodha ya wachezaji nyota 10 waliofanya vizuri, Samatta pia anashika nafasi ya tatu katika orodha ya washambuliaji waliong’ara kwenye mashindano hayo.
Samatta ambaye katika mashindano hayo amecheza mechi tatu kwa dakika 263, akifunga mabao matatu, kutoa pasi moja iliyozaa bao, akipiga jumla ya mashuti sita huku matano kati ya hayo yakilenga lango, amemzidi nyota wa Arsenal, Aubameyang.
Mshambuliaji huyo amecheza mechi mbili akitumia dakika 143, akifumania nyavu mara mbili bila kupiga pasi iliyozaa bao huku akipiga mashuti tisa, matano tu yakilenga lango na anashika nafasi ya 22.
Lacazette ametoa pasi moja ya bao bila kufunga, katika mechi mbili alizocheza dakika 28 tu huku akiwa hajapiga shuti, wakati Giroud katika mechi mbili alizocheza dakika 100, hajafunga wala kupiga pasi iliyozaa bao, akipiga mashuti manne tu ambayo miongoni mwa hayo, mawili tu ndiyo yalilenga lango.
Morata aliyecheza mechi mbili kwa dakika 170, akifunga moja bila kupiga pasi ya mwisho, amepiga mashuti 15 na yaliyolenga lango ni matatu tu.
Welbeck aliyewahi kucheza Manchester United, amefunga mabao mawili pasipo kupiga pasi ya mwisho kwenye dakika 261 alizocheza katika mechi tatu, akipiga mashuti matano huku matatu tu ndiyo yalilenga lango.
Katika hali ya kushangaza, Wakati Samatta akishika nafasi ya 10 katika orodha ya wacheza 100 bora wa mashindano ya Europa hadi sasa, Aubameyang anashika nafasi ya 22 huku Welbeck, Lacazette, Morata na Giroud wote wameshindwa kuwemo kwenye kundi la nyota hao.
Samatta ‘amewapiga’ bao washambuliaji hao baada ya kupata pointi 4711, Aubameyang (4015), Lacazette (1578), Welbeck (2308), Giroud (943) na Morata (1447).
Ukiondoa washambuliaji hao, pia Samatta amewafunika mastaa wengine akina Eden Hazard, Cesc Fabregas, Pedro Rodriguez, Mesut Ozil, Victor Moses, N’Golo Kante na Henrikh Mikhitaryan.

Comments

Popular posts from this blog

Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!