BMT yataka uchaguzi Yanga




Dar es Salaam. Baraza la Michezo Taifa (BMT), limeitaka Klabu ya Yanga kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi ikiwemo ya Mwenyekiti Yusuf Manji.
Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Alex Nkeyenge alisema Yanga inatakiwa kufanya uchaguzi ndani ya mwezi huu baada ya klabu hiyo kukaa muda mrefu bila ya kuwa na mwenyekiti.
Nkeyenge alisema kuwa licha ya juhudi za Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kumshawishi Manji kurejea katika nafasi hiyo, lakini kiongozi huyo hakuonyesha kuwa tayari kuiongoza Yanga.
Alisema uongozi wa Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupanga tarehe ya uchaguzi mwezi huu kujaza nafasi hiyo.
“Tunawataka wanachama wajiandikishe upya kwenye matawi ili kupata orodha ya wanachama wanaotakiwa kupiga kura za uchaguzi wa kujaza nafasi zote zilizoachwa wazi ndani ya wiki tatu kuanzia sasa,”alisema Nyeyenge.
Pia aliagiza Kamati ya Uchaguzi ya TFF kusimamia uchaguzi na kuweka bayana kuwa nafasi ya mwenyekiti inatakiwa kujazwa kwa kuwa Manji ameshindwa kuonyesha dhamira ya kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Baada ya Manji kujiuzulu mwaka jana, wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji waliojiondoa ni Hashim Abdallah, Salum Mkemi, Omari Said. Pia Makamu Mwenyekiti Clement Sanga alitangaza kujiuzulu wadhifa huo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, alisema klabu itatoa taarifa rasmi baada ya kupata barua kutoka BMT.
Awali, Yanga ilitangaza kufanya uchaguzi Novemba 26 kujaza nafasi za wajumbe na Makamu Mwenyekiti huku ikiendelea kumtambua Manji kama mwenyekiti wa klabu hiyo.

Comments

Popular posts from this blog

Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!