Majembe manne kumrithi Okwi



KADI mbili za njano alizopata straika Emmanuel Okwi, zimewanyima usingizi Waganda kuelekea mchezo wao wa kutafuta tiketi ya kufuzu michuano ya Afcon dhidi ya Cape Verde na sasa benchi lao la ufundi linaumiza kichwa kujua nani atakuwa mbadala wake.
Okwi ambaye kwa sasa ni kama roho ya timu hiyo ya Taifa ya Uganda kutokana na kufunga mabao muhimu, ataukosa mchezo huo utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii Uwanja wa Namboole, nchini humo.
DIMBA Jumatano liliwasiliana na mwandishi wa habari nguli kutoka nchini Uganda, David Isabirye, ambaye alisema kutokuwepo kwa Okwi kunawafanya wachezaji wanne kuandaliwa ili mmoja avae viatu vyake.
“Ni kweli Okwi hatakuwepo mchezo huo dhidi ya Cape Verde wa Jumamosi inayokuja kutokana na kutumikia adhabu ya kadi mbili za njano, anaweza akacheza leo (jana) mchezo wa kirafiki dhidi ya Nigeria tu,” alisema.
Alisema mmoja wa wachezaji hao anayeweza angalau kuziba pengo la Okwi, ni Milton Karisa anayechezea Klabu ya Mouloudia Club D’Oujda ya nchini Morocco na hii ni kutokana na kasi aliyonayo.
Mwingine ambaye anaweza kujaribu viatu vya Okwi, ni Moses Waiswa anayechezea Vipers Sports Club, ambapo katika mchezo dhidi ya Taifa Stars, alicheza kama winga na inadaiwa kwamba kiwango chake kinaongezeka siku hadi siku.
Yupo pia Edrisa Lubega anayeichezea SV Ried ya nchini Austria, ambaye pia anatajwa kwamba kasi aliyonayo inaweza kuwasahaulisha Waganda umuhimu wa Okwi.
Mwandishi huyo alisema mbali na hao, pia Allan Katerega ambaye misimu kadhaa iliyopita alikuwa akiwindwa na vigogo Simba na Yanga, anaweza kufiti nafasi hiyo kutokana na kazi nzuri anayoifanya katika timu yake ya Cape Town City ya Afrika Kusini.
Idadi hiyo inaonyesha jinsi Mganda huyo anayekipiga katika klabu ya Simba hivi sasa alivyokuwa na umuhimu katika kikosi cha timu yake ya Taifa anayoitumikia kwa kipindi kirefu.

Comments

Popular posts from this blog

Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!