Simba ya MO ni balaa tupu
IN SUMMARY
- Katika mechi zao 11 walizocheza mpaka sasa, Simba imevuna jumla ya mabao 23 ikiwa ndiyo klabu yenye mabao mengi zaidi kuliko nyingine zinazoshiriki ligi hiyo kwa msimu huu yenye timu 20.
MASHABIKI wa Simba kwa sasa wana kila sababu ya kunenepa. Wakonde wana stresi gani bwana, wakati mkwanja wa bilionea wao, Mohammed ‘MO’ Dewji unaendelea kuwapa raha duniani kutokana na timu yao kukimbiza Bongo.
Ikiwa katika mbio za kutetea taji lao la Ligi Kuu Bara walilolitwaa msimu uliopita baada ya kulisotea kwa miaka mitano, Simba ya sasa ni moto ikiwakimbiza wapinzani wao, ikiwamo Yanga iliyowatesa kwa miaka kadhaa walipokuwa ovyo.
Kama hujui ni kwamba safu ya ushambuliaji ya Simba kwa sasa inathibitisha jeuri ya fedha ya timu yao kulingana na watani zao wa Yanga ambao, wanaishi maisha ya kuungaunga kwa sasa kutokana na hali yao ya uchumi kuyumba.
Kiwango kikubwa cha fedha ambacho Simba imekuwa ikitumia kulipa mishahara nyota wake kimeonekana kuzaa matunda kwa safu ya ushambuliaji na kuwapiga bao mastraika wa watani zao wa jadi Yanga.
Timu zote mbili zinaonekana zinavuna kutokana na kile ambacho zimepanda kupitia mishahara ya nyota hao, kwani Simba inayotumia fungu kubwa la fedha kulipa mishahara nyota wae imeonekana kunufaika zaidi kulinganisha na Yanga.
Inakadiriwa kiasi cha Sh 28.5 milioni kinatumika kila mwezi kwa ajili ya kulipa mishahara ya washambuliaji wake sita tu, huku matunda yakionekana kwa timu hiyo kuwa vinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara mpaka sasa.
Katika mechi zao 11 walizocheza mpaka sasa, Simba imevuna jumla ya mabao 23 ikiwa ndiyo klabu yenye mabao mengi zaidi kuliko nyingine zinazoshiriki ligi hiyo kwa msimu huu yenye timu 20.
Katika mabao hayo 23 yaliyotupiwa kambani na Simba, mabao 18 yamefungwa na washambuliaji asilia ilionao huku mengine matano yakifungwa na nyota wa nafasi nyingine.
Miongoni mwa nyota wanaochuma kiasi kikubwa cha fedha ndani ya kikosi cha Simba kupitia mshahara wanaolipwa, Meddie Kagere anaonekana ametendea haki zaidi fedha hizo akiwa amefunga mabao saba.
Kagere anayelipwa kiasi cha Dola 5,500 (Sh 12 milioni) hadi sasa ameshapachika mabao saba akifunga dhidi ya Prisons, Mbeya City, Stand United, Alliance na Ruvu Shooting.
Ukiondoa Kagere, nyota mwingine anayevuna mkwanja mrefu Msimbazi ni Emmanuel Okwi ambaye inakadiriwa analipwa mshahara wa Dola 3,500 (zaidi ya Sh7 milioni) naye akiwa ametupia kambani mabao saba pia. Mabao hayo akiyafunga dhidi ya African Lyon, Stand United, Alliance na Ruvu Shooting.
Ukiondoa nyota hao wa kigeni, nahodha John Bocco anayetajwa kuvuna Sh 4 milioni kwa mwezi na Adam Salamba anayevuta Sh 1.5 milioni nao wametendea haki mishahara ya Simba kwa kupachika mabao mawili kila mmoja.
Katika orodha hiyo ya washambuliaji wa Simba ni Mohammed Rashid na Marcel Kaheza wanaotajwa kulipwa Sh 1.5 kila mmoja ndio wameshindwa kutendea haki fedha za Simba wanazolipwa kama mishahara kwa kutofunga bao hata moja.
HUKO YANGA SASA
Wakati Simba wakionekana kupata faida ya kile walichokiwekeza kwenye mishahara ya washambuliaji wake, upande wa pili ambao ni Yanga wenyewe wameonekana kupata kile wanachostahili kutokana na fungu dogo wanalotoa.
Inakadiriwa kuwa Yanga hutumia kiasi cha Sh 15milioni pekee kwa ajili ya kulipa mishahara kwa nyota wake watano washambuliaji asilia.
Yanga katika Ligi Kuu msimu huu mpaka sasa imefunga mabao 17 katika mechi zao 10, mabao 9 kati ya hayo yakifungwa na mastraika hao, huku mengine yakitupiwa nyavuni na nyota wa nafasi nyingine wakiwamo mabeki Andrew Vincent ‘Dante’ na Kelvin Yondani na mawinga, Mrisho Ngassa na Deus Kaseke. Heritier Makambo anayelipwa Dola 1,500 (Sh 3 milioni), amefunga mabao manne, Amissi Tambwe anayechukua Dola 2,000 (zaidi ya Sh 4 milioni) amefunga mabao mawili, huku Ibrahim Ajibu anayetajwa kulipwa Sh 4 milioni akifunga matatu na kutoa pasi za mabao tisa.
Mastraika Yohana Mkomola na Mateo Anthony wanaodaiwa kulipwa Sh 2.5 milioni, hawajafunga bao lolote mpaka sasa, wakizidiwa na viungo Feisal Salum ‘Fei Toto’, Rafael Daud na Jaffar Mohammed waliotupia kila mmoja bao moja moja.
MBELGIJI SAFI
Kutokana na kasi ya nyota wa Simba katika kutupia, Kocha Patrick Aussems amesema ni faraja kwani anaona mambo yanaenda kama anavyotaka japo anataka kasi iongezeke zaidi.
Alisema anaridhishwa na kasi ya upachikaji mabao kwa washambuliaji wake na anaamini wanatoa msaada mkubwa kwa timu.
“Jambo kubwa ni kufunga na kama unavyoona, Bocco, Okwi na Kagere wote wanafanya hivyo na sasa hivi Salamba naye ameanza kufunga japo anachezeshwa kwa muda mdogo,” alisema Aussems na kuongeza;
“Naamini hili ni jambo zuri kwa timu hasa ukizingatia hatukuwa tukifunga mabao mengi katika mechi za mwanzoni,” alisema.
Comments
Post a Comment