MKUDE, CHAMA WAPEWA KAZI MAALUM KUIUA MBABANE
SIMBA ipo katika maandalizi makali ya mechi yake ya Jumatano ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mbabane Swallows kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, kocha Mbelgiji, Patrick Aussems amewapa kazi maalumu viungo wake wawili, Jonas Mkude na Mzambia, Cletus Chama.
Akuzungumza na Championi Jumatatu, Mkude alisema kuwa Aussems amefikia hatua hiyo baada ya kukamilisha uchunguzi wake dhidi ya Mbabane Swallows.Alisema katika uchunguzi huo alibaini kuwa Mbabane wapo vizuri sehemu ya kiungo, ndiyo maana akaamua kuwapatia kazi maalumu.
“Kwa sasa tunaendelea kujifua vilivyo ili tuweze kuwa fiti tayari kwa kuifanya kazi hiyo ambayo kocha ametupatia, ni matumaini yangu kuwa hatutamwangusha kocha, tutaifanya kama anavyotaka.
“ Kazi yenyewe hiyo kwa sasa siwezi kuisema ila kwa yeyote atakayekuja uwanjani siku hiyo ataiona,” alisema Mkude ambaye hucheza nafasi ya kiungo mkabaji akishirikiana vilivyo na Mghana, James Kotei.
Kwa upande wake Chama yeye hucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji anayetokea pembeni sawa na Shiza Kichuya. Wakati huohuo, Mbabane wanatarajiwa kutua nchini leo Jumatatu saa 2:00 kwa ajili ya mchezo huo.
SWEETBERT LUKONGE, Dar es Salaam
Comments
Post a Comment