AMUNIKE KAA MGUU SAWA, SISI WATANZANIA NI WABRAZILI
MWAKA 2001, timu ya taifa ya Brazil ilikuwa kwenye hatikati ya kukosa michuano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kutokana na mwenendo wa kusuasua wa timu hiyo.
Inajulikana wazi kati ya nchi yenye presha kubwa katika mchezo wa soka kuliko zote ni Brazil, kuna sababu kubwa kama tatu hivi, kwanza ni vipaji vingi walivyonavyo, pili ni wingi wa watu wa taifa hilo (inakaridiwa wapo zaidi ya watu milioni 200) na tatu ni kuwa kila mtu ni kocha kwenye taifa hilo.
Kuna wakati ilifika hatua unaweza kupanga vikosi vitano vya taifa la Brazil na vyote vikawa bora na vinaweza kufika fainali ya Kombe la Dunia.
Juni 2001, Luiz Felipe Scolari aliteuliwa kuwa kocha wa taifa hilo, presha ilikuwa kubwa, alianza mchezo wa kwanza vibaya kwa kufungwa na Uruguay bao 1-0, baada ya hapo akaendelea vizuri na mwisho akatangaza kumuacha kikosini ‘Mungu’ wa soka wa wakati huo kwa Wabrazili, Romário.
Ilikuwa ngumu kwa Wabrazili kumuelewa kwa kuwa waliamini Romario ndiye kila kitu kwao. Baadhi ya mashabiki wakamwambia anapoenda kushiriki katika Kombe la Dunia, ahakikishe anarejea na taji, kinyume na hapo apande ndege apitilize anapopajua na siyo kurejea Brazil.
Scolari aliuvaa moyo wa paka, akaenda na kubeba kombe akarejea kifua mbele, chuki yote ikapotea na akaonekana ni shujaa.
Stori hiyo nimeisimulia ili iendane na kile ambacho nitakizungumza hapa, Kocha wa Taifa Stars, Mnigeria, Emmanuel Amunike amekuwa na misimamo kama ya Scolari kwa kiasi fulani licha ya kuwa ana muda mfupi tangu awe bosi wa timu hiyo.
Katika mchezo dhidi ya Uganda kuwania kufuzu Afcon 2019, aliwaacha wachezaji wa Simba kwa kile kilichoelezwa kuwa walichelewa kuripoti kambini, japokuwa baadaye ilibainika kulikuwa na tatizo la mawasiliano na ndiyo maana kiongozi mmoja akachukuliwa hatua, Amunike hakutaka kubadili maamuzi, akashikilia msimamo wake.
Taifa Stars ikaambulia matokeo ya 0-0 ikiwa na wachezaji wengi ambao awali hawakuwemo katika mipango.
Stars ilipoenda kucheza na Cape Verde, Amunike pia akafanya maamuzi ya kumuacha pembeni beki mkongwe Kelvin Yondani kwa sababu anazozijua yeye, pengo likaonekana na timu ikapoteza kwa mabao 3-0.
Aliporejea nchini akarekebisha makosa na timu ikapata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya haohao Cape Verde. Mchezo wa juzi dhidi ya Lesotho, Stars ilionekana kuwa na kikosi ambacho wengi walikishangaa na ndiyo maana hata baada ya kupoteza lawama zimekuwa nyingi kwa kocha huyo.
Sikuwepo kambini lakini pia kilichotokea baadaye ni kuwa kulikuwa na maneno mengi kuhusu mvurugano kambini.
Nikukmbushe kitu kimoja, wiki chache wakati akiwa hotelini anapoishi, Amunike aliwahi kuulizwa na gazeti hili sababu za kutomuita kikosini Ibrahim Ajibu wa Yanga ambaye kwa miezi ya hivi karibuni amekuwa akionyesha kiwango cha juu na kwa kuwa soka halichezwi chumbani kila mtu ameliona hilo.
Sehemu ya majibu yake alisema hivi: “Nani Ajibu? Ndiyo nani huyo? Kwani mchezaji yuko peke yake? Wapo wengine wanaofaa zaidi yake na kuna wachezaji wengi tu ninaoweza kuwaita siyo lazima yeye.”
Kauli hiyo ilinishangaza kidogo na sikutegemea kutolewa na mtu mwenye uzoefu mkubwa katika soka kama Amunike ambaye kama ni ile hali ya kuwa ‘profesheno’ ilikuwa sehemu ya maisha yake.
Hilo likapita na sasa kuna tetesi kuwa alivurugana na baadhi ya wachezaji kambini na ndiyo maana wengine hakuwapanga.
Katika soka, Tanzania licha ya kuwa hatuna mafaniko makubwa lakini ukweli ni kuwa tuna tabia kama za Wabrazili, tunajua kumpa mtu presha, tunajua kumpamba mtu tukiamua na tunajua kumvuruga tena sana kama tukiamua.
Rekodi za ukocha zinaonyesha Amunike pamoja na kucheza soka kwa kiwango cha juu hajawahi kukutana na kazi kubwa na yenye presha kama hii, kwa kuwa alikuwa ni kocha wa timu za vijana au msaidizi miaka ya nyuma.
Kuajiriwa kuwa kocha wa Stars ni wazi ni cheo chake cha kwanza kikubwa tangu aanze majukumu ya ukocha, yawezekana akaifanya kuwa sehemu ya kujifunza kwake lakini wale mliopo karibu naye mfikishieni ujumbe kuwa sisi Watanzania ni Wabrazili, akitaka atufunge mdomo afanye yale aliyoyafanya Scholari.
Comments
Post a Comment