SIMBA KUWEKA HISTORIA UCHAGUZI WA VIONGOZI WAPYA LEO
WANACHAMA wa klabu ya Simba wataweka historia leo (Jumapili) watakapoingia kwenye uchaguzi mkuu kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Historia hiyo itaandikwa kwa Simba kwani wanakwenda katika mfumo mpya wa kuendesha klabu kutoka katika nguvu ya wanachama mpaka kwenye mfumo wa mabadiliko ambao klabu itaendeshwa kwa uwekezaji wa mfumo wa hisa ambao utaongozwa na atakayekuwa muwekezaji wake, Mohammed Dewji ‘MO’.
MO alishinda zabuni ya mchakato wa Simba na atamiliki klabu kwa asilimia 49 akitoa Sh. bilioni 20 huku wanachama wakimiliki asilia 51 na wajumbe saba ambao watachaguliwa katika uchaguzi wa leo wataingia katika bodi ya wakurugenzi wa timu hiyo.
Wajumbe hao saba ambao watachaguliwa leo watakuwa wawakilishi wa wanachama wa Simba kwa kupigania maslahi yao wakati kikao cha bodi kikiwa kinafanyika, ikimaanisha MO naye atakuwa na wawakilishi wake saba ambao watangia katika kikao hiko kupigania maslahi yake.
Simba walifanya uchaguzi mara ya mwisho miaka minne nyuma na walimchagua Rais Evance Aveva na makamu wake Nyange Kaburu ambao kwa sasa wapo rumande sambamba na wajumbe wengine ambao waliendesha timu kwa muda wote huo.
Baada ya Aveva na Kaburu kukabiliwa na mashitaka mahakamani yaliyotokana na nafasi zao uongozi wa Simba ulikaimishwa chini ya Kaimu Rais Salim Abdallah ‘Try Again’ na Makamu Rais Iddy Kajuna ambaye ameingia tena katika uchaguzi wa mwaka huu akiwania nafasi ya ujumbe.
Kabla ya uchaguzi, Simba wameanza na mkutano mkuu uliotegemewa kuanza saa 2:30 asubuhi na kumalizika saa 6:00 mchana ambapo wanachama wangepewa mapumziko ya saa moja kisha saa 7:00 wangeanza mchakato mzima wa uchaguzi.
Katika uchaguzi huo kulitegemewa kuwepo masanduku matatu ambapo la kwanza lingekuwa la nafasi ya mwenyekiti ambalo anatakiwa kupigiwa kura za ‘ndiyo’ au ‘hapana’ kutokana na kwamba yuko peke yake katika nafasi hiyo.
Anayewania uenyekiti ni Swedy Nkwabi baada ya mgombea mwenza Mtemi Ramadhani kujiondoa kwa madai ya kubanwa na majukumu mengi ya kifamilia, hivyo anatakiwa kupata asilimia 51 na kama zitakuwa chini ya hapo kura zitapigwa tena.
Sanduku lingine ambalo wanachama walitarajiwa kupiga kura ni la wagombea wawili wa kike ambao ni Jasmine Badar na Asha Baraka wote wakiwania katika nafasi ya ujumbe na ambaye atapata kura nyingi ndiyo atashinda katika nafsi hiyo.
Sanduku la mwisho litakuwa la wagombea wa kiume ambao wanatakiwa kupatikana wajumbe sita kati ya wajumbe 15 watakaowania nafasi hiyo ya ujumbe. Katika Sanduku hili wajumbe sita ambao watapatikana kuna mmoja anatakiwa kuwa na elimu wa shahada (degree) na wengine kuwa na elimu isiyopungua ya kidato cha nne kama katiba inavyosema.
Wagombea wote ni ni Swedy Nkwabi — nafasi ya mwenyekiti — wengine ni nafasi ya wajumbe ambao ni Asha, Jasmine, Selemani Omari, Patrick Rweyemamu, Abubakari Zebo, Juma Pinto, Said Tully, Mwina Kaduguda, Ally Suru, Alfred Aliya na Christopher Kabalika.
Wengine ni Abdallah Migomba, Selemani Harubu, Mohamed Wandi, Zawadi Kadunda, Iddy Kajuna na Hussein Kitta.
Comments
Post a Comment