ZAHERA ATAJA ALIPO MAKAMBO
BAADA ya mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo raia wa DR Congo kudaiwa kutoweka klabuni hapo huku taarifa zake zikiwa hazieleweki alipo, kocha wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera amemuibua mshambuliaji huyo.
Makambo mwenye mabao 11 akiwa kinara wa ufungaji kwenye Ligi Kuu Bara, inadaiwa aliondoka Yanga takribani wiki mbili zilizopita.
Tangu aondoke nchini, mawasiliano yake na viongozi wa klabu hiyo hayakuwa mazuri hali ambayo ilizua maswali mengi.
Mshambuliaji huyo ambaye jana Jumanne alikosekana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao timu yake ilicheza dhidi ya Mwadui FC katika Uwanja wa Taifa, Dar, anatarajiwa kuwepo katika mchezo ujao dhidi ya Stand United, mwishoni mwa wiki hii.
Zahera raia wa DR Congo kama ilivyo kwa Makambo, kipa wa timu hiyo, Klaus Kindoki na kiungo, Papy Tshishimbi, ameliambia Championi Jumatano kuwa: “Makambo alienda DR Congo na anarudi Jumatano (leo).”
Awali uongozi wa Yanga ulipishana juu ya taarifa za kutoweka kwa Makambo ambapo ofisa habari wa klabu hiyo, Dismas Ten alisema: “Makambo alienda kwao DR Congo na atarudi siku yoyote. Kuhusu kutopatikana kwa mawasiliano yake ni ishu tu za kimtandao.”
Wakati Ten akisema hivyo, msaidizi wake, Godlisten Anderson ‘Chicharito’, alisema: “Mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo ataukosa mchezo dhidi ya Mwadui kutokana na kuwa na kadi tatu za njano. Hajatoweka kama taarifa za kwenye mitandao zinavyodai.”
Comments
Post a Comment