SPURS V MAN UNITED…VITA YA KIBABE KILA KONA



Wachezaji wa Manchester United 
MANCHESTER United na Tottenham Hotspur zinatazamiwa kuvaana leo Jumapili kwenye mechi kali ya Ligi Kuu England itakayopigwa kwenye Uwanja wa Wembley jijini London.
Wachambuzi wa soka wanaamini kuwa mchezo huo ndio utakaopima uwezo wa kocha wa muda wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer.

Solskjaer ameshinda mechi tano mfululizo tangu alipopewa nafasi hiyo ingawa wataalamu wa soka wanadai ilikuwa dhidi ya timu ndogo.

Kitendo cha kukabiliana na Spurs kwenye Uwanja wa Wembley kitakuwa kipimo kikubwa cha Mnorway huyo.
Solskjaer anafahamu fika kuwa akishinda mchezo huu atakuwa ametengeneza mazingira mazuri ya timu yake kutinga kwenye nne bora ya Ligi Kuu England na kupata tiketi ya kucheza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kama mchezo huu ungechezwa mwezi mmoja nyuma, timu ya Pochettino ingepewa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na jinsi Manchester United ilivyokuwa inacheza soka mbovu chini ya kocha wa zamani, Jose Mourinho.

Kitendo cha Manchester United kushinda mechi tano mfululizo hivi karibuni kimeongeza uzito wa mchezo huu.
Ushindi kwa Spurs utawasogeza karibu na vinara wa ligi ambao ni Liverpool lakini wakipoteza mchezo huu basi watapunguza kwa kiasi kikubwa matumaini yao ya kutwaa ubingwa.
Mchezo huu unatazamiwa kuwa wa kuvutia kutokana timu zote mbili kuundwa na wachezaji wenye kipaji cha hali ya juu,.
Kutakuwa na vita kali baina ya mastaa wa timu hizo muda wote wa mchezo huo kiasi cha kufanya mchezo huu kuwa mkali.
• Toby Alderweireld v Marcus Rashford
Marcus Rashford kwa sasa ndio anacheza kama straika wa kati wa Manchester United, ambapo kwa kiasi kikubwa atavaana na beki wa kati wa Tottenham, Toby Alderweireld.
Alderweireld ni kati ya mabeki bora wa Ligi Kuu England na amegomea kusaini mkataba wa kuendelea kuchezea timu hiyo.
Hivi sasa timu nyingine zinataka kumsajili beki huyo wa timu ya taifa ya Ubelgiji.
Alderweireld ni beki anayetumia akili na mzuri wa mipira ya juu, ambapo hucheza na Jan Vertongen kama mabeki wa kati wa Tottenham.
Alderweireld, hata hivyo, anatakiwa kuwa makini wakati atakapokabiliana na straika wa Manchester United, Rashford .
Rashford amekuwa moto tangu timu imekuwa chini ya Solskjaer na amekuwa akichezeshwa kama straika wa kati.
Straika huyo anaogopewa kutokana na umahiri wake wa kupiga chenga na mbio zake zimekuwa zikiwapa wakati mgumu mabeki wa timu pinzani.
• Sissoko/Winks v Paul Pogba
Kiungo mkabaji wa Tottenham Hotspur, Eric Dier atakosa mchezo huu kutokana na kuwa majeruhi na Moussa Sissoko na Harry Winks ndio wataziba pengo lake.
Sissoko ana uwezo wa kucheza winga wa kulia na beki kiungo wa kati.
Winks naye katika siku za karibuni amekuwa anapata nafasi kwa kiasi kikubwa kutokana na kuumia kwa Moussa Dembele na Victor Wanyama.

Sissoko watakuwa na kibarua kizito dhidi ya staa wa Manchester United, Paul Pogba ambaye siku za karibuni amekuwa anatisha.
Pogba alikosa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Reading kutokana na kuwa majeruhi, ambapo sasa anatazamiwa kuwa fiti dhidi ya Spurs.
Mfaransa amekuwa anacheza kwa furaha tangu ujio wa Solskjaer, ambapo amekuwa akipanda mbele kusaidia mashambulizi na pia kufunga mabao.
• Harry Kane vs Victor Lindelof
Straika wa Tottenham Hotspur, Harry Kane ni mfungaji hatari wa mabao, ambaye hatakiwa kuachiwa upenyo kwenye eneo la timu pinzani.
Hakuna beki wa timu za Ligi Kuu England anayependa kucheza dhidi ya straika huyo wa England.
Kane pia ni mzuri katika kumiliki mpira, ambapo kama mshambuliaji wa kati husaidiana na mwenzake Dele Alli.
Pia ni mzuri wa mipira ya juu, kiti ambacho kinafanya iwe vigumu kumchunga wakati wa mipira ya kona na faulo.

Manchester United imekuwa na wakati mgumu kutengeneza safu ya ulinzi katika msimu huu wa 2018-19.
Mourinho alijaribu kutengeneza kombinesheni ya mabeki Phil Jones, Chris Smalling, Eric Bailly, na Marco Rojo, ambapo ilishindikana na kumfanya kuanza kufikiria kusajili mabeki wengine.
Hata hivyo, tangu ujio wa Solskjaer, beki wa kati, Victor Lindelof amekuwa anafanya vizuri tofauti na timu hiyo ilipokuwa chini ya Mourinho.
Lindelof ana kipaji cha kumiliki mpira na ana uwezo mkubwa wa kupokonya mipira kwa hiyo mapambano yake na Kane yatakuwa kivutio kikubwa.
LONDON, England

Comments

Popular posts from this blog

Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!