JOELLE BUKURU… MRUNDI WA SIMBA ANAYETAMANI KUICHEZEA TWIGA STARS




LIGI ya Wanawake inazidi kuunguruma kwenye viwanja tofauti huku vipaji kibao vikishuhudiwa kutoka katika timu 12 zinazoshiriki ligi hiyo inayozaminiwa na kinywaji cha Serengeti Lite.

Simba Queens ni miongoni mwa timu shiriki kunako ligi hiyo na tayari imeshashuka dimbani katika michezo mitano na kuvuna jumla ya pointi 13.
Nyuma ya mafanikio hayo yupo mchezaji nyota wa Kikosi hicho, Joelle Bukuru ambaye anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji.
Mrundi huyo huu ni msimu wake wa kwanza ndani ya ligi hiyo akiwa na jezi ya Simba. Amekuja nchini na mwenzake anayeitwa Aisha Djafar.
Joelle Bukuru (kushoto mwenye mpira) akifanya yake.
Bukuru ni miongoni mwa nyota ambao Jumapili iliyopita waliisaidia Simba kuibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Yanga Princess katika mwendelezo wa ligi hiyo, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Karume, Dar.
Championi Jumatano limefanya mahojiano na nyota huyo juu ya maisha yake ya kwa jumla.
“Naitwa Joelle Bukuru, nimezaliwa Burundi katika familia ya watoto watatu. Mimi ndiye mkubwa nikiwa na pacha wangu anaitwa Abubakari, na kuna mdogo wetu.

Nani alikuleta Tanzania?
“Nahodha wetu Mwanahamisi Omary ndiye aliyenishawishi kuja kucheza soka Tanzania, aliniona kwenye mechi ya timu zetu za taifa, akakubali uwezo wangu na akanishawishi kuja huku.

Kwa nini uliichagua Simba?
“Ni timu ambayo naona inaweza kuishi kwa muda mrefu tofauti na timu za kule kwetu huwa hazikai muda mrefu kutokana na kukosa malezi imara.
Huu ni msimu wako wa ngapi katika soka la ushindani?
“Msimu wangu wa tatu nacheza kwa sababu kule Burundi nimecheza misimu miwili na hapa Tanzania ni msimu wangu wa kwanza.

Tofauti kati ya ligi ya hapa na Burundi ipoje?
“Ligi ya hapa ni nzuri na yenye ushindani mkubwa, lakini pia kuna wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa tofauti na kwetu Burundi.
“Burundi ligi yake ni nyepesi sana, watu hawachezi kwa kujituma, lakini huku wachezaji wanapambana na kuonyesha uwezo mkubwa sana.

Maisha ya hapa kwa jumla unayaonaje?
“Naishi vizuri sana kwa sababu ni moja ya nchi nzuri, tunaishi kwa upendo sana na wachezaji wenzangu pamoja na viongozi wa timu.

Katika nafasi unayocheza, ni nani anakupa changamoto?
“Bado sijaona kwa sababu mimi najiamini sana na huwa najitahidi kucheza kwa kujituma sana, sisemi kama hakuna wachezaji wazuri ila mimi naamini ni zaidi.

Umecheza na Yanga Princess, umewaonaje?
“Wapo vizuri ila sisi tulikuwa bora zaidi yao na ndiyo maana tuliwafunga mabao saba, ila wanapaswa kuongeza juhudi zaidi kwa sababu wachezaji wao wengi hawajitumi.

Vipi unalipwa mshahara?
“Ndiyo, ila siwezi kusema ni bei gani, watu wajue tu kuwa ninalipwa mshahara kila mwezi na hata kuja hapa nilisajiliwa na pesa, sikuja tu.

Ukiambiwa ubadili uraia ucheze timu ya taifa ya Tanzania utakubali?
“Kwa hilo siwezi kusema kwa sababu nimeshachezea timu ya Burundi ila kama inaruhusiwa kubadili uraia na kuchezea nchi nyingine, nitafanya hivyo, hakuna shida.

Wazazi wako wanakusapoti vipi kwenye maisha yako ya soka?
“Wananisapoti kwa vitu vingi sana na siku zote wananiambia lazima niongeze juhudi na nidhamu kama nataka kufika mbali.

Malengo yako kwenye soka yapoje?
“Malengo yangu ni kuipa Simba ubingwa wa msimu huu ili niweze kupata njia ya kwenda kucheza soka Ulaya,” anasema Joelle.

Comments

Popular posts from this blog

Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!