WACHEZAJI YANGA WAMPINGA MWINYI ZAHERA



Mwinyi Zahera
MUDA mfupi baada ya wachezaji wa Yanga kumaliza mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar, kocha wa timu hiyo, Mwinyi Zahera akatangaza kumvua unahodha beki Kelvin Yondani jambo lililowashangaza baadhi ya nyota wa kikosi hicho.

Yondani alikabidhiwa kitambaa cha unahodha mkuu na aliyekuwa beki nguli kikosini humo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alistaafu miezi michache iliyopita na sasa ni meneja wa timu hiyo. Zahera ambaye amekuwa hataki utani linapokuja suala la nidhamu, ameweka wazi kuwa amemvua
Yondani kitambaa hicho na kumkabidhi mshambuliaji mwenye kipaji, Ibrahim Ajibu.
Chanzo cha Zahera kumvua unahodha Yondani ni kutokana na utoro mazoezini ambapo alichelewa kuripoti baada ya muda waliopewa wa mapumziko ya siku tano kupita na hakutoa taarifa yoyote. Zahera alisema: “Kuanzia leo (jana) mimi kama kocha wa Yanga nimeamua kumtoa unahodha Kelvin Yondani na atabaki kuwa mchezaji wa kawaida kama wachezaji wengine.

“Nilitoa siku tano za mapumziko kwa wachezaji wote na siku ya sita walitakiwa kuwa mazoezini lakini yeye aligoma kufika mazoezini na wala hakutoa taarifa yoyote. “Mtu ambaye alikuwa ni nahodha alipaswa kuonyesha mfano mzuri kwa wenzake, kuanzia leo (jana) nimemchagua Ajibu kuwa nahodha mpya wa Yanga,” alisema Zahera. Hata hivyo jambo hilo lilipokelewa kwa namna tofauti na wachezaji wa timu hiyo huku wengi wakidai kuwa kocha huyo hakumtendea haki kwani alitoa adhabu bila kumsikiliza.

“Kusema kweli hakumtendea haki Yondani, kabla ya kuchukua maamuzi hayo alipaswa kumsikiliza kwanza ndipo achukue hatua, yule ni binadamu na inawezekana alikuwa na matatizo ambayo pengine yalisababisha akajisahau kutoa taarifa. “Hakika wachezaji wengi hilo limetushangaza sana, Yondani ni kiongozi ambaye kila mmoja wetu kazi yake anaijua anapaswa kumsikiliza kwanza,” alisema mmoja wa wachezaji hao.

Championi Jumamosi lilimtafuta Yondani azungumzie ishu hiyo ambapo alipatikana na kuweka wazi kuwa alipatwa na matatizo na atayaweka wazi mara baada ya kukutana na kocha Zahera. “Sijapata taarifa rasmi lakini, nimechelewa kujiunga na wenzangu siyo kwa makusudi bali nilikuwa na matatizo ambayo nitayaweka wazi kwa kocha mwenyewe baada ya kukutana naye.
“Binafsi ninaomba msamaha kwa kilichotokea kwa maana ya kutotoa taarifa mapema kabla ya yeye kufikia maamuzi hayo,” alisema Yondani.

Comments

Popular posts from this blog

Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!