KISA SIMBA… KOCHA AS VITA AMPIGIA SIMU ZAHERA
MUDA mfupi tu baada kuona amepangwa kundi moja na Simba SC kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika,Kocha Mkuu wa AS Vita Club ya DR Congo, Florente Ibengé, fasta akainua simu na kumpigia Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera.
AS Vita ambayo ipo mjini Kinshasa, DR Congo, imepangwa kundi moja na Simba kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Timu zingine zilizopo kwenye kundi la la D ni Al Ahly ya Misri na JS Saoura ya Algeria.
Simba itaanza karata yake kwa kucheza na JS Saoura anayochezea Mtanzania Thomas Ulimwengu, Jumamosi ijayo na mechi ya kwanza dhidi ya AS Vita itakuwa Januari 19, kule DR Congo na watarudiana jijini Dar, Machi 15, mwaka huu.
Kama hujui ni kwamba Kocha Ibenge ndiye bosi wa Zahera pale kwenye Timu ya Taifa ya DR Congo, yaani Ibenge ni kocha mkuu na Zahera ni msaidizi wake.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Zahera ambaye huu ni msimu wake wa kwanza kuinoa Yanga, alisema kuwa mara baada ya Caf kupanga makundi hayo alipigiwa simu na bosi wake huyo na kumueleza juu ya ujio wa kuja kucheza na Simba kwenye ligi hiyo.
“Ibengé nafanya naye kazi kwenye timu ya taifa akiwa kama bosi wangu na baada kupangwa makundi tu na kuona watacheza na Simba alinipigia simu, akacheka na kuniambia kwamba wanakuja Tanzania kucheza na Simba, nimemkaribisha.
“Kiukweli hakuniuliza jambo lolote juu ya Simba ipo vipi au ina wachezaji gani, ila najua lazima ataniuliza tu siku yoyote kabla hawajakutana,” alisema Zahera.
Comments
Post a Comment