RASMI SONSO AMALIZANA NA YANGA SC
YANGA imelamba dume! Unaweza kusema hivyo baada ya kumalizana na beki wa kati mwenye kiwango cha juu wa Lipuli FC, Ally Mtoni ‘Sonso’, sasa ataungana na kikosi hicho kesho Jumapili.
Yanga ilianza mbio za kumuwania mlinzi huyo ambaye alionyesha uwezo mkubwa kwenye mechi ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyocheza dhidi ya Lesotho katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Mataifa Afrika.
Championi Jumamosi ambalo lipo mkoani Iringa, lilizungumza na mlinzi huyo ambaye alikuwa na nyota wenzake wa Lipuli kwa mara ya mwisho kabla ya kwenda kuanza maisha mapya pale Yanga jijini Dar.
Sonso ambaye ni mrefu na amefuga rasta kichwani mwake, amelihakikishia Championi Jumamosi kuwa amemalizana na Yanga na anachosubiri kwa sasa ni viongozi wa Lipuli na Yanga kumalizana kwa ngazi ya uongozi ambao tayari wameanza mazungumzo.
“Nimeshamalizana na Yanga, nilikuwa nasubiri viongozi wangu wamalizane na Yanga ili niweze kuondoka. Wameniambia Jumapili ndiyo nitaungana na Yanga.
“Nimejisikia vizuri kutokana na dili hilo kukamilika, kwa muda mrefu nilikuwa natamani nicheze timu kubwa hapa nchini kama Yanga.
“Nafurahi kwanza kwenda kucheza na Yondani (Kelvin) na naamini kombinesheni yetu itakuwa nzuri. Kwa muda mrefu nilikuwa natamani nicheze naye timu moja.
“Binafsi nafasi yangu uwanjani ni beki wa kati na pale Yanga kuna wachezaji wengi wazuri kwenye nafasi hiyo, lakini nitafanya juhudi kubwa kuhakikisha nacheza kikosi cha
kwanza,” alisema Sonso.
Hata hivyo, Championi linafahamu kwamba Lipuli ipo njiani kumalizana na Yanga kwenye usajili wa Sonso ambapo dau lake ni Sh milioni 50.
Comments
Post a Comment