STRAIKA WA MIL 100 SIMBA MGUU NDANI, NJE



DIRISHA dogo la usajili linafunguliwa Novemba 15 mwaka huu, tayari mambo ni moto kwani ndani ya Simba, mshambuliaji wa timu hiyo, Mohammed Rashid huenda akaonyeshwa mlango wa kutokea.

Rashid alisajiliwa na Simba msimu huu akitokea Prisons kwa dau la Sh mil 30 na mshahara wake unaonyesha analipwa Sh Mil 3 hivyo ukijumlisha kwa miaka miwili aliyosaini, jumla ataingiza Sh 102m.

Simba imejaza washambuliaji wengi kwenye kikosi chao kiasi cha wengine kukosa nafasi ya kucheza mpaka sasa hivyo Rashid amekuwa akitajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji watakaoondolewa na atarudishwa Prisons kwa mkopo kwani kocha Patrick Aussems hajavutiwa na uwezo wake.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumamosi limezipata zimedai kuwa, kuna uwezekano mkubwa klabu hiyo kutoongeza mchezaji yeyote kwenye dirisha dogo zaidi ya kuangalia wale ambao hawapati nafasi sana na kuwatoa kwa mkopo.

“Ishu ya usajili katika dirisha dogo kuna uwezekano mkubwa wa kutoongeza mchezaji yeyote zaidi ya kuwatoa kwa mkopo baadhi yao katika timu walizotoka.
“Mpaka sasa kocha anasema kikosi chake kimekamilika kina wachezaji wengi na wazuri kwa kila nafasi ila kuna baadhi hawana sifa za kuitumikia Simba hivyo hao itabidi watafutiwe timu nyingine wakakuze uwezo wao.

“Mmoja kati ya wachezaji hao ni Mohammed Rashid kwani kwa jinsi hali ilivyo itakuwa ni vigumu kwake kupata nafasi ya kucheza mbele ya Emmanuel Okwi, John Bocco, Meddie Kagere, Adam Salamba, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga, Claytous Chama, Haruna Niyonzima na Said Ndemla ambao wote wanacheza nafasi ambazo pia amekuwa akicheza,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Aussems alisema: “Muda wa usajili bado haujafika kwa hiyo siwezi kuzungumzia ishu ya usajili kwa sasa, tusubiri muda ukifika kila kitu kitajulikana.”

Comments

Popular posts from this blog

Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!