MABAO YA OKWI, CHAMA YAMPONZA KICHUYA



USISHANGAE kuona kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya akianzia benchi huku akiwapisha mastaa Mganda, Emmanuel Okwi na Mzambia, Claytous Chama wakicheza nafasi zake kutokana na ukame wa mabao alionao.
Kichuya hadi hivi sasa amefunga bao moja pekee akiwa amecheza michezo nane tangu Ligi Kuu Bara imeanza, akianza katika kikosi cha kwanza tofauti na mchezo uliopita na Alliance FC ambao alikaa benchi.

Wakati Kichuya akifunga bao moja, wenzake Meddie Kagere na Okwi wamefunga manne kila mmoja huku Chama akifunga mawili katika michezo miwili mfululizo pamoja na kuonyesha uwezo wa juu.
Kichuya anatarajiwa kupata ugumu wa namba baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems kufanya mabadiliko ya haraka katika kikosi chake kwa kuwahamisha Okwi na Chama kucheza viungo wanaotokea pembeni namba 7 na 11 nafasi inayochezwa na kiungo huyo.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Aussems alisema anataka kuwa na washambuliaji wenye uwezo wa kufunga mabao na siyo kingine, hivyo atatoa nafasi kwa wachezaji wenye uchu wa kufunga wanapolifikia goli la wapinzani wao.
Aussems alisema hajutii kumtoa mchezaji kwenye kikosi chake cha kwanza na kumuingiza mwingine aliye kwenye benchi kama ilivyokuwa kwa Kichuya ambaye mchezo na Alliance alikuwepo amekaa benchi.

“Mimi hivi sasa nguvu na akili zangu ninazielekeza kwenye ufungaji pekee ambazo nimezianza kwenye mchezo huu na Alliance, ni kuhakikisha timu yangu inapata ushindi wa mabao mengi na siyo kitu kingine.
“Hivyo, kama ikitokea mshambuliaji anakosa umakini kwa kushindwa kutumia nafasi anazozipata katika kufunga mabao, ni lazima nitamtoa katika kikosi changu na hiyo ndiyo sera yangu hivi sasa na kikubwa ninataka kuona timu yangu ikipata ushindi wa mabao mengi.

“Ninafurahia kumuona kiungo kama Chama akifunga mabao katika michezo miwili mfululizo akitokea pembeni na Okwi naye, hivyo ndivyo ninavyotaka kama unakumbuka mchezo na Stand United wachezaji wangu Kichuya na Kagere walishindwa kutumia nafasi nyingi za wazi katika kufunga mabao na ndiyo sababu ya kuwaweka benchi, kikubwa ninataka wajifunze kupitia kwa wenzao,” alisema Aussems.

Comments

Popular posts from this blog

Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!