SIMBA SC YAIFANYIA UMAFIA YANGA SC
IMBA imeingia kwenye anga za Yanga, baada ya kocha Patrick Aussems kumfukuzia beki anayewaniwa na vinara hao wa Ligi Kuu Bara. Wekundu wa Msimbazi, juzi Jumamosi walitupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa 4-1 na TP Mazembe mjini Lubumbashi, na sasa hasira zao wanazihamishia kwenye Ligi Kuu Bara ili wapate nafasi nyingine ya kucheza Ligi ya Mabingwa mwakani.
Tayari uongozi wa Simba umeshaanza mikakati ya kuwasaka wachezaji wakubwa ili wawe na nguvu zaidi msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa, na wanataka wavuke hatua ya robo fainali ambayo wamekomea msimu huu.
“Tumejifunza vitu vingi hadi hatua hii ambayo tumefikia na kutolewa. Tumeona kwamba ili usonge mbele kwenye hatua kubwa ni lazima uwe na wachezaji wenye viwango vikubwa na sisi kwa mwakani tutalifanyia kazi hilo,” alisema jana Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori.
Baada ya mechi hiyo ya ambayo ilichezwa huko Lubumbashi nchini DR Congo na Simba kufungwa mabao 4-1, kocha mkuu Patrick Aussems aliutaka uongozi wa timu hiyo kuanza mara moja harakati za kumwania beki wa kati wa AS Vita na timu ya taifa ya DR Congo, Bangala Litombo kwa ajili ya kuimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Inaelezwa kuwa Aussems amefikia hatua hiyo kutokana na kutofurahishwa na makosa yaliyofanywa na baadhi ya mabeki wake wa kati katika mchezo huo na kujikuta akiutaka uongozi huo kuhakikisha unamnasa beki huyo.
Kitendo hicho cha kumtaka Litombo, kinaweza kumuingiza Aussems katika vita kubwa ya usajili na Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye pia hivi karibuni aliweka wazi kuwa anamtaka Litombo kwa ajili ya kuimarisha safu yake ya ulinzi, baada ya msimu huu kukabiliwa na changamoto nyingi.
Kama vile haitoshi, Zahera alidai kuwa licha ya ugumu atakaokumbana nao katika kuiwania saini ya beki huyo, lakini anaamini kuwa kwa sababu ana mahusiano mazuri na viongozi wa timu hiyo, basi jambo hilo linaweza kusaidia akampata kirahisi.
Habari za kuamini kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumatatu limezipata zimedai kuwa, Aussems alimuona Litombo na kuvutiwa na uwezo wake baada ya timu hiyo kupambana na AS Vita huko Kinshasa DR Congo lakini pia jijini Dar es Salaam katika mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Kwa hiyo kocha ameutaka uongozi kuhakikisha wanaanza haraka iwezekanavyo kumwania beki huyo ambaye pia ni tegemeo kubwa katika timu yake ya Vita na ile ya Taifa ya DR Congo.
“Ishu hiyo alikuwa ameshaizungumza siku nyingi na uongozi lakini baada ya makosa ya safu ya ulinzi katika mechi
yetu ya marudiano ya TP Mazembe ikambidi asisitize jambo hilo lifanyike haraka iwezekanavyo,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Aussems hakuwa tayari kusema chochote zaidi ya kudai: “Muda wa usajili haujafika kwa hiyo kwa sasa siwezi kusema chochote ila jambo kubwa ni kwamba tumeondolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na tayari tumerudi nyumbani kuendelea kupambana katika ligi kuu ili tuweze kufanya vizuri katika mechi zetu zote za ligi hiyo zilizobakia
Comments
Post a Comment