AJIBU AONDOLEWA RASMI YANGA…KISA KIPO HAPA
HABARI za moto zinazosambaa kwa kasi kwenye ulimwengu wa michezo ni kuwa inadaiwa Klabu ya Yanga imeamua kuchukua maamuzi magumu na kumuondoa kikosini nahodha wake, Ibrahim Ajibu kutokana na kuwepo kwa taarifa kadhaa tata juu yake.
Inaelezwa kuwa sababu kubwa ya kuchukuliwa kwa maamuzi hayo ni kudaiwa kuwa kuna ‘mgomo baridi’ ambao staa huyo amekuwa akiufanya kiasi cha kuhusishwa kuwa ni njia ya yeye kushinikiza aongezewe mkataba. Takribani wiki tatu sasa, Ajibu amekuwa nje ya kikosi hicho ikielezwa kuwa amekuwa akisumbuliwa na majeraha, jambo ambalo limekuwa gumu kuaminika kwa mashabiki na baadhi ya viongozi wa Yanga wakiamini kuna sababu nyuma ya kukosekana kwake uwanjani.
Chanzo cha habari kimelieleza gazeti hili hivi: “Tayari viongozi wetu wameshamshtukia Ajibu juu ya janja yake ya kugoma kuisaidia timu katika michezo inayoendelea ili ashinikize kupewa mkataba mpya kwa kiwango anachotaka yeye, la sivyo aachwe na aende kuitumikia Simba msimu ujao.
“Hivyo, viongozi wanaendelea kumfuatilia na kama hatashiriki michezo miwili ijayo basi atapigwa ‘stop’ hata ya kufanya mazoezi na kikosi chetu. “Hakuna jambo ambalo linakwaza kama kumuona mchezaji ambaye aliaminiwa na kocha kwa malengo makubwa ya kumjenga ili aje kuisaidia timu, lakini yeye haoni hilo na kwamba amekuwa akifanya mambo ya kitoto kiasi cha kumkatisha tamaa hata kocha mwenyewe.
“Anasema anaumwa lakini timu ikirudi Dar es Salaam kutoka mikoani anajiunga nayo kufanya mazoezi, kocha ameamua kutoa mawazo kwake na ameshaanza kuandaa safu mpya pasipo kumuwazia tena yeye,” kilisema chanzo hicho.
Kuhusu kutua Simba Tetesi za kuwaniwa na Simba ambayo imekuwa ikijipanga vizuri tangu kuanza kwa uwekezaji wa bilionea, Mohamed Dewji ‘Mo’, zimeshika kasi lakini hakuna upande ambao umekuwa tayari kufunguka japokuwa gazeti hili linafahamu tayari kuna mazungumzo baina ya Simba na Ajibu na alishasaini mkataba wa awali.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten alipoulizwa kukosekana kwa Ajibu kwenye timu alisema: “Anasumbuliwa na maumivu ya nyonga ndiyo yamesababisha aondolewe kikosini na siyo kitu kingine.
“Niwatoe hofu Wanayanga kuwa Ajibu bado yupo na ana mkataba na klabu, atajiunga na timu itakaporejea Dar.” Kuhusu tetesi za kuwaniwa na Simba alisema: “Kuna tetesi nyingi juu ya wachezaji wetu muhimu, mashabiki waungane kuichangia timu yao kupitia kampeni ya kocha wetu Zahera (Mwinyi).” Alipotafuta Daktari wa Yanga, jana mchana, Edward Bavu hakupokea simu hadi tunaingia mtamboni.
Comments
Post a Comment