Zahera afumua kikosi chote Yanga
KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera ameamua kufumua kikosi chote huku akisisitiza kwamba hafanyi mambo kufurahisha mashabiki. Zahera amekwenda mbali na kusisitiza kwamba hata katika mechi ya kirafiki leo Jumapili dhidi ya AFC Leopards hakuna hata mchezaji mmoja aliyecheza Moshi dhidi ya Polisi Tanzania atakayeanza. Katika mechi dhidi ya Polisi juzi Ijumaa Yanga ilifungwa mabao 2-0 huku ikianzisha sura nyingi mpya.
Zahera amekwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba hata kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Township Rollers hakuna mchezaji yoyote aliyecheza dhidi ya Polisi ataanza. Kikosi cha kwanza kilichoanza dhidi ya Polisi kilikuwa na Ramadhani Kabwili,Mustafa Seleman,Gustava Saimon,Ally Ally,Kelvin Yondani,Abdulaziz Makame,Maybin Kalengo,Feisal Salum,David Molinga na Deus Kaseke.
Kocha huyo anayezungumzia Kiswahili cha lafudhi ya Kicongo amesisitiza kwamba anakifanyia mabadiliko makubwa kikosi hicho ili kupata ubora anaouhitaji tayari kwa mechi dhidi ya Township pamoja na ligi. Amesema kuwa tangu kwenye mechi dhidi ya Kariobangi Jijini Dar es Salaam amekuwa akipangua kikosi na atafanya pia mabadiliko makubwa leo Jijini Arusha ingawa Spoti Xtra linajua kwamba kikosi cha leo ndio kitakachoanza dhidi ya Township.
Katika mazoezi ya jana Jumamosi wachezaji waliofanya ni wale waliocheza mechi dhidi ya Polisi huku wengine wakipumzishwa hotelini, hiyo inamaanisha kwamba ndiyo watakaoanza mechi ya leo ingawa Yondani huenda akaongezwa.
Kikosi hiki huenda kikaanza leo; Metacha Mnata, Paul Godfrey, Ally Sonso, Lamine Moro, Yondani, Tshishimbi, Mapinduzi Balama,Mohammed Banka, Patrick Sibomana, Juma Balinya na Sadney Urikhob Zahera amesisitiza kwamba kabla ya kucheza na Township atakuwa na kikosi imara cha kwanza ambacho kitacheza soka kwenye ubora na hadhi ya Yanga ndio maana amekuwa akitoa nafasi kwa wachezaji wote kila mmoja atumie muda wake na kujitambua kabla hajafanya maamuzi.
“Kwenye hizi mechi za kirafiki sichezeshi kikosi kamili, ndio maana hata tukipoteza sioni kama ni tatizo sana. “Kinachotakiwa ni wachezaji kuonyesha uwezo wao kwenye mechi hizo, kama huwezi kunionyesha uwezo katika mechi za kirafiki utaonyesha wapi? Kwa kupata nafasi kwenye kikosi cha Yanga mwaka huu unapaswa kuonyesha utofauti
mkubwa, ushindani ni mkubwa,”alisisitiza Zahera.
KUONDOKA JUMANNE Keshokutwa Jumanne,Yanga itakwenda nchini Botswana kujiandaa na mchezo wa marudiano wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers.
Hata hivyo, Yanga itaondoka nchini bila ya kuwa na baadhi ya nyota wake wapya wa kigeni kutokana na kukosa vibali vya Caf. Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Dismas Ten ameliambia Spoti Xtra kuwa wachezaji hao ambao ni Farouk Shikalo, Mustapha Seleman pamoja na David Molinga wataikosa mechi hiyo kwa sababu mpaka sasa bado
hawajapata leseni zao kutoka CAF.
“Wachezaji hao wataikosa kwa sababu mpaka sasa leseni zao kutoka CAF bado hatujazipata. “Kama tutasonga mbele katika michuano hiyo hatua inayofuata ndiyo tutawatumia, kilichosababisha mpaka sasa leseni zao zichelewe ni kutokana na hati zao za uhamisho wa kimataifa (ITC) kuchelewa kuzipata, kwa hiyo hatuna jinsi, kama tutafanikiwa kusonga mbele basi katika hatua inayofuata tutakuwa nao,” alisema Ten. 10:00 Yanga itacheza kwa mara ya kwanza jijini Arusha leo saa 10 jioni dhidi ya AFC Leopards ya Kenya katika mechi ya kirafiki.
Comments
Post a Comment