Msimu Mpya: Samatta Afanya Maangamizi Ubelgiji



 NAHODHA wa timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta amefunga mabao matatu (hat-trick), katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza nchini Ubelgiji dhidi ya Waasland-Beveren.

Samatta aliiongoza klabu ya KRC Genk kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo huo uliochezwa juzi, kwenye Uwanja wa Freethielstadion, mjini Beveren.

Mshambuliaji huyo alifunga mabao hayo, dakika za 53, 66 na 86, huku bao jingine likifungwa na Joseph Paintsil dakika ya 21.

Samatta anakuwa mshambuliaji wa tatu kufikisha mabao manne, baada ya kucheza michezo minne ya ligi hiyo msimu huu, wengine ni Dieumerci Mbokani wa Royal Antwerp na David Okereke wa Club Brugge.

Huo ni mwanzo mzuri kwa Samatta ambaye msimu uliopita aliimaliza nafasi ya pili kwenye chati ya wafungaji bora wa ligi hiyo , akiwa na mabao 23, mabao mawili nyuma ya Hamdi Harbaoui wa Zulte Waregem aliyechukua kiatu cha ufungaji bora.

Samatta sasa amefikisha mabao 66, katika mechi ya 160 za mashindano yote, tangu amejiunga na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika ligi ya Ubelgiji pekee, amefunga mabao 51 kwenye mechi 126, Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, Super Cup baio moja na Europa League, mechi 24 mabao 14.

Comments

Popular posts from this blog

ALIYEIPELEKA TAIFA STARS AFCON 1980 AFUNGUKA WALIVYOPAMBANA – VIDEO

Simba Vs Azam: Mtakula za Kutosha!