MATOLA: TULIENI NIWAONYESHE NAMNA SIMBA INAVYOFUNGWA
LICHA ya Simba kushinda mechi zake zote za hivi karibuni kwa kuanza na Mwandui 3-0, akafuata Mwarabu 1-0, African Lyon 3-0, Yanga 1-0 na Azam FC 3-1, kocha wa Lipuli, Selemani Matola amesema atawafunga Simba.
Simba itacheza kesho na Lipuli mchezo wa ligi ikiwa ni kiporo kwenye Uwanja wa Samora huku rekodi zikionyesha kwamba tangu msimu wa 2017/2018 Lipuli ilipopanda daraja, hakuna hata timu iliyoonja ushindi kwa mwenzake.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Matola alisema amewatazama wapinzani wake kwa ukaribu na kujua udhaifu wao, hali ambayo imemfanya aamini kwamba kesho atavunja rekodi iliyowekwa kwa timu hizi mbili.
“Siyo mechi rahisi, tumejipanga kamiligado, mechi tatu zimepita hakuna aliyebeba pointi tatu kwa mwenzie, sasa sisi tuna hamu sana kuwa wa kwanza kubeba pointi tatu nyumbani.
“Najua Simba ni timu nzuri na ina kitu cha kipekee kwa sasa kutokana na ushindi ambao wamepata hivi karibuni, lakini hilo halitupi taabu kwa kuwa bado ni Simba walewale ingawa wana kitu kipya walichonacho, tutawazuia nyumbani na kuvunja rekodi ile ya michezo yetu mitatu tuliyocheza nao,” alisema Matola.
Katika michezo hiyo mitatu ambayo walicheza nao msimu wa 2017/18 wakiwa nyumbani Simba walilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Samora, mchezo wa marudiano Lipuli walilazimisha sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa. Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu huu, zilitoka suluhu Uwanja wa Taifa.
Comments
Post a Comment